Mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegie ashambuliwa na mpenziwe

Tom Mathinji
1 Min Read
Mwanariadha wa Uganda Rebecca Cheptegei

Mwanariadha wa Uganda  Rebecca Cheptegie, amelazwa hospitalini nchini Kenya baada ya kuchomwa moto na mpenzi wake, kulingana na maafisa wa polisi.

Cheptegie, aliyeshiriki mashindano yal Olimpiki yaliyokamilika hivi majuzi nchini Ufaransa, alichomeka asilimia 75, baada ya mpenzi wake kumchoma kwa mafuta ya petroli, kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Shambulizi hilo lilitekelezwa Jumapili alasiri nyumbani kwao katika kaunti ya Trans Nzoia. Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 33, yuko katika hali mbaya, huku akipokea matibabu katika hospitali moja mjini Eldoret.

Maafisa hao wa polisi walisema kuwa mpenzi huyo wa Cheptegie aliyetambuliwa kuwa Dickson Ndiema Marangach, pia alijeruhiwa na moto huo.

Wazazi wa mwanariadha huyo waliotoka nchini Uganda kumtembelea mwanao, walisema Cheptegie alinunua nyumba na shamba nchini Kenya, ili iwe rahisi kwake kufanya mazoezi.

Share This Article