Maafisa wa polisi wanachunguza kifo cha mwanariadha mstaafu Samson Kandie, aliyeuawa na watu wasiojulikana nyumbani kwake kaunti ya Uasin Gishu.
Kulingana na Kamanda wa polisi Kaunti ya Uasin Gishu Benjamin Mwanthi aliyethibitisha kisa hicho, alisema Kandie alishambuliwa nyumbani kwake katika mtaa wa Elgon View.
“Alishambuliwa na watu ambao ni kwamba walikuwa wanamsubiri nyumbani kwake, tunachunguza kisa hicho,” alisema Mwanthi.
Alisema washambuliaji hao walichukua rununu yake, pekee wakati wa tukio la Alhamisi usiku, ambalo limesababisha mshtuko na hofu miongoni mwa wakazi. Mkuu huyo wa polisi alisema uchunguzi unaendelea.
”Tunawatafuta washukiwa hao, ili wachukuliwe hatua za kisheria,” aliongeza afisa huyo mkuu wa polisi.
Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 53, aliyesherehekewa kwa ushindi wake katika mbio za marathoni za Sapporo mwaka 2002 na Vienna mwaka 2004, alipatikana ameshambuliwa na polisi wamesema alikuwa amefungwa mikono na miguu.
Wanariadha katika eneo hilo wakiongozwa na Ezekiel Kemboi, wameeleza masikitiko yao kuhusiana na mauaji ya Kandie, na kuihimiza serikali kuimarisha usalama kwa wanariadha wa humu nchini.
Kemboi alisema eneo hilo limepoteza wanariadha wengi, siku za hivi majuzi lakini hakuna hatua zozote za maana zimechukuliwa kuwalinda wanariadha .