Kevin Wyre ambaye ni mwanamuziki ametangaza kifo cha mtoto wa kiume wa mwanamuziki mwenzake Nazizi Hirji.
Kwenye taarifa aliyochapisha mitandaoni kwa niaba ya Nazizi, Wyre alielezea kwamba mtoto huyo kwa jina Jazeel Hirji wa umri wa miaka mitatu, aliaga dunia Disemba 25, nchini Tanzania.
Aliendelea kusema kwamba mvulana huyo alifariki kutokana na ajali iliyotokea kwenye hoteli moja nchini humo ambapo walikuwa wamekwenda kwa likizo.
Mwili wa Jazeel Hirji ulizikwa Disemba 26 hapa Nairobi kulingana na mipangilio ya dini.
Wanahabari na umma kwa jumla wanaombwa kumpa Nazizi na familia yake muda ili kuomboleza mwanao kwa utulivu.
Aliahidi kwamba taarifa ya kina itatolewa baadaye.