Mwanamuziki Joe Mopero afariki

Marion Bosire
2 Min Read

Mwanamuziki wa Kenya Joe Mopero amefariki.

Binti yake aitwaye Joy Mopero ndiye alitoa taarifa kuhusu kifo cha babake akielezea kwamba kilisababishwa na mshtuko wa moyo.

Joy aliendelea kuelezea kwamba mzee huyo gwiji wa muziki alikata roho saa 12 na dakika 45 jioni Jumamosi Oktoba 25, 2025 katika hospitali ya Aster Healthcare, ambako alikimbizwa baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Mopero, ambaye jina lake halisi ni Joseph Kariuki, alizaliwa katika eneo la Kipkabus, katika Kaunti ya Uasin Gishu, miaka ya 1960, kabla ya familia yake kuhamia Thika.

Akiwa mwanafunzi katika Shule ya Upili ya Equator, wenzake walimpa jina la utani “Joe Mopero” kutokana na jinsi alivyokuwa akiimba kwa mtindo unaofanana na ule wa mwanamuziki wa Kongo Mopero wa Maloba.

Mopero Maloba alifahamika sana kwa mtindo wake wa Cavacha uliopendwa sana nchini Kenya wakati huo.

Joe Mopero aliwahi kuimba na bendi kadhaa za Kenya na Kongo zilizokuwa na makao yao Nairobi.

Katika miaka ya mapema ya 1990, aliunda bendi yake mwenyewe iliyojulikana kama Zambezi Band, na kupitia bendi hiyo akarekodi wimbo maarufu “Heri Nirudi Nyumbani”.

Wimbo huo ulipata umaarufu mkubwa mara moja na hadi leo, zaidi ya miongo mitatu baadaye, bado unapendwa na mashabiki wengi.
Hadi hivi karibuni, Mopero aliendelea kutumbuiza na bendi yake katika kumbi mbalimbali ndani na nje ya jiji la Nairobi.

Alikuwa ametoa pia nyimbo kadhaa mpya. Mashabiki wake watamkumbuka kwa sauti yake nzito ya baritone na ustadi wake wa kipekee wa uchezaji gitaa.

Website |  + posts
Share This Article