Maafisa wa polisi katika kaunti ya Murang’a wameanzisha msako wa mwanamume mmoja mwenye umri wa makamo anayedaiwa kuwaua wanawe wawili na kutoroka.
Evans Kang’ethe ambaye ni baba wa watoto wawili, Samuel Irungu mwenye umri wa miaka saba na Briton Mwangi mwenye umri wa miaka mitatu, anasemekana kutekeleza mauaji hayo usiku wa kuamkia leo baada ya ugomvi kuibuka kati yake na mkewe.
Wakazi wenye ghadhabu wametishia kumuua Kang’ethe aliye na umri wa miaka 28 wakimtaja kuwa kijana asiyekuwa na tabia nzuri mbali na kuwa mraibu wa dawa za kulevya.
Akizungumza na wanahabari, mamake mzazi Anna Njeri alilalama kuwa mwanawe amekosa adabu, hatua ambayo imesababisha ugomvi wa mara kwa mara kati yake na mkewe.
Njeri aliongeza kuwa wiki iliyopita, kijana huyo alimrushia babake mzazi makonde akimshurutisha kumgawia shamba.
Ameiomba serikali kufanya kila juhudi na kumkamata kijana huyo akiongeza kuwa hata wao wanahofia maisha yao.
Wakazi sasa wanawaomba vijana kutojihusisha na uraibu wa dawa za kulevya na kuzitaka mamlaka kumtia mbaroni mshukiwa kwa tuhuma za mauaji.