Mwanamume mwenye umri wa miaka 59 nchini Mexico, amefariki kutokana na aina ya homa ya ndege – H5N2, ambayo haijawahi kurekodiwa kwa binadamu hapo awali.
Aidha mamlaka nchini humo imeondolea mbali wasiwasi kuhusu virusi hivyo, ikisema hakuna jamaa wa karibu wa mwathiriwa huyo ameambukizwa homa hiyo.
Haijulikani aliambukizwa vipi virusi hivyo, ingawa kumekuwa na visa katika baadhi ya mashamba ya kufuga kuku nchini Mexico.
Maambukizi kama haya wakati fulani yanaweza kupita kutoka kwa wanyama hadi kwa wanadamu.
Mwanaume huyo alikuwa na changamoto nyingine za kiafya ambazo huenda zilimfanya kuwa hatarini.
Alikuwa amelazwa kwa wiki kadhaa kabla ya kuugua homa na kushindwa kupumua kutokana na mafua ya ndege, kulingana na maafisa.
Shirika la Afya Ulimwenguni na mamlaka zingine hufuatilia aina za mafua, kama hii, ambayo inaweza kuwa na mabadiliko na kuwa tishio.