Mchekeshaji na muunda maudhui mitandaoni nchini Kenya Tabitha Gatwiri amefariki.
Kifo chake kimetangazwa mitandaoni na waigizaji wenzake wanaosema kwamba aliugua kwa muda mfupi kabla ya kukumbana na mauti.
Mwili wa mwendazake uliopatikana kwenye nyumba yake kwa sasa umehifadhiwa katika makafani ya hospitali ya chuo kikuu cha Kenyatta.
MC Bull alimwomboleza Gatwiri kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii akielezea kwamba mwezi uliopita walijadiliana kuhusu kuandaa maudhui pamoja.
“Siamini haupo tena. Ni mwezi uliopita tulijadili kuhusu kuandaa maudhui ya pamoja. Sina raha, sina maneno ya kuzungumza. Talanta yako itakoswa. Mwenyezi Mungu aipe familia yako nguvu wakati huu mgumu.” aliandika MC Bull.
Mwigizaji mwingine maarufu kama Shiphira ambaye amewahi kushirikiana na Garwiri katika kazi zao za mitandaoni naye amemwomboleza akisema hana maneno ya kusema.
“Hii nayo inauma. Tabitha Gatwiri lala salama hadi tutakapokutana tena.” aliandika Shiphira chini ya picha ya marehemu.
Siku chache zilizopita, Gatwiri alichapisha bango la kuomba mchango la dada ya mwigizaji wa mitandaoni Bena wa malines ambaye alikuwa afanyiwe upasuaji.