Shambulizi la angani lililotekelezwa na Israel kwenye kambi ya Nuseirat katika ukanda wa Gaza limesababisha vifo vya mwanahabari wa Palestina Ahmed Al-Louh na maafisa watano wa usalama wa Palestina.
Al-Louh alikuwa akifanya kazi kama mpiga picha wa kampuni ya Al Jazeera na nyingine za habari na aliuawa Jumapili katika shambulizi lililolenga kituo cha ulinzi katikati mwa Gaza.
Mashambulizi mengine yalitekelezwa na Israel katika maeneo mbali mbali ya Gaza ambapo wapalestina 28 waliuawa. Al-louh ndiye mwanahabari wa tatu ameuawa katika muda wa saa 24 huko Gaza.
Alikuwa anaendelea na kazi alipokumbana na mauti na alikuwa amevaa mavazi ya kikazo pamoja na kofia ya chuma.
Usimamizi wa kampuni ya Al Jazeera umekashifu mauaji yake na kuyataka mashirika ya haki za binadamu na yombo vya habari kukemea hatua ya Israel ya kuua wanahabari, hatua ya kukwepa kuwajibika na kuhakikisha haki.
Al-Louh amekuwa akiangazia vita vya Israel katika ukanda wa Gaza tangu vilipoanza Oktoba 2023, na amekuwa akishirikiana na maafisa wa ulinzi wa Palestina.
Kituo kikuu cha habari huko Gaza kimeripoti pia kwamba mkuu wa huduma za dharura katika kambi ya Nuseirat, Nedal Abu Hjayyer, naye aliuawa kwenye shambulizi la Jumapili.
Zaki Emadeldeen, mmoja wa wahudumu hao wa dharura aliambia wanahabari kwamba shambulizi hilo lilifanywa wakati wote walikuwa kambini.
Alielezea kwamba huduma yao ni ya kibinadamu na haihusiki na siasa kwa vyovyote. Huwa wanashughulika wakati wa vita na hata wa amani kuhakikisha watu wako salama.
Jeshi la Israel limesema kwamba linachunguza shambulizi hilo.