Usimamizi wa Shule ya Upili ya Kenya High, umetangaza kutoweka kwa mmoja wa wanafunzi wake, katika hali ya kutatanisha.
Kupitia kwa taarifa siku ya Alhamisi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Edith Koech, alisema kuwa mwanafunzi huyo Joy Wanjiri Gathigia alichukuliwa shuleni humo na kaka yake saa nne asubuhi na kupelekwa hadi kituo cha matatu cha 2NK ambako aliabiri gari la kuelekea Nyeri.
Kulingana na taarifa hiyo, mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu alitarajiwa kushuka katika kituo kabla ya Nyeri mjini, lakini dereva wa gari hilo alidokeza kuwa Joy badala yake aliamua kushukia Nyeri mjini.
“Baadhi ya vitu vyake vilipatikana karatina, lakini hajulikani aliko,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Shule hiyo imetoa wito kwa yeyote aliye na habari kumhusu mwanafunzi huyo, kupiga ripoti katika kituo cha polisi kilicho karibu, au kufahamisha shule hiyo.