Polisi nchini Uganda wamemkamata mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17, kwa madai ya kuwasafirisha vijana 170.
Polisi walisema walimkamata mwanafunzi huyo wa shule ya upili tarehe 18 mwezi Septemba, katikati mwa Uganda.
Polisi wanasema kuwa mwanafunzi huyo aliwaweka vijana 170 katika nyumba ya mwanamke mwenye umri wa miaka 28, wakati wakisubiri usafiri hadi mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambako mwanafunzi huyo alikuwa amewaahidi kazi.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi la Uganda lilisema siku ya Jumanne kwamba mpango huo wa usafirishaji haramu wa binadamu ni ulaghai.
“Alipohojiwa, mwanafunzi alikiri kwamba alitaka kuwanyang’anya waathiriwa pesa kwa kutumia jina la Kampuni ya Humble nchini Kenya kama siri.
“Hakukuwa na uhusiano na kampuni hiyo na tangazo la kazi kwa wahudumu, watengenezaji kahawa na wahudumu wa maduka makubwa nchini Kenya lilikuwa bandia,” Jeshi la Polisi la Uganda lilisema katika taarifa.
Gazeti la kibinafsi la Daily Monitor la Uganda limeripoti kuwa 98 kati ya waathiriwa walimlipa mwanafunzi huyo shilingi 100,000 za Uganda ($26; £21) kila mmoja huku wengine wakilipa shilingi 50,000 kila mmoja.
Mwanafunzi huyo bado hajaombwa kujibu mashtaka dhidi yake.