Msanii Peter Wangudi maarufu kama Mwana Mtule hatimaye ameondoka kwenye hospitali ya kitaifa ya Kenyatta.
Haya yanajiri yapata mwezi mmoja tangu aliporuhusiwa kuondoka na madaktari kwani alikuwa amepata nafuu ila hakuwa amekamilisha malipo ya matibabu na hivyo hangeondoka.
Yapata wiki saba zilizopita, Mwana Mtule alitangaza kwamba alitiliwa sumu kwenye chakula wakati wa sherehe fulani aliyokuwa amealikwa huko Rongai kaunti ya Kajiado.
Anasema jamaa fulani ambaye hakumfahamu alimpigia simu akamtaka afike atumbuize kwenye hafla hiyo wito ambao aliitikia hata ingawa malipo yalikuwa ya chini mno.
Kulingana naye, tajiri wake alikubali kumlipa shilingi elfu tatu naye akaridhia akafanya kazi na baadaye akala chakula ambacho baadaye kilibainika kuwa na sumu.
Alipelekwa hospitalini na marafiki wake ambapo amekuwa hadi leo baada ya mchekeshaji na mwanaharakati Eric Omondi kuongoza mchango mitandaoni na kufanikisha malipo ya bili ya shilingi elfu 450.
Mwana Mtule anashukuru wote waliomchangia ili kumwezesha kurejelea maisha yake ya kawaida.