Jackson Marucha mwalimu wa shule ya msingi ya Riang’ombe katika kaunti ya Nyamira ameshtakiwa kwa kosa la kujaribu kuua kufuatia hatua yake ya kuchapa mwanafunzi viboko 104.
Marucha alitiwa mbaroni mwezi Machi mwaka 2023 kufuatia kisa hicho ambapo alimchapa mwanafunzi wa gredi ya nne wa umri wa miaka 9 viboko vingi na kumsababishia majeraha kwenye makalio.
Alifikishwa mahakamani Ijumaa Julai 19, 2024 ambapo mahakama ilifahamishwa kwamba mwanafunzi husika aliachwa na majeraha ukiwemo mgando wa damu uliotishia kuumiza moyo wake vibaya na hata labda ungesababisha kifo.
Mwanafunzi huyo alikuwa amepoteza sare yake ya shule hatua iliyomgadhabisha mwalimu Marucha na akaamua kumshambulia kwa viboko.
Baada ya kugundua alichokuwa amekifanya, mwalimu huyo alijaribu kumficha mhasiriwa kwenye bweni lakini akagunduliwa na kukimbizwa hospitalini.
Marucha alikwenda mafichoni lakini maafisa wa usalama walifanikiwa kumpata na kumtia mbaroni kwa kosa hilo.
Upande wa mashtaka ulitaka masktaka yawe jaribio la kuua ikitizamiwa madhara ambayo mwalimu Marucha alimsababishia mtoto huyo.
Utetezi bado haujatoa taarifa zake kwenye kesi hiyo ambayo inaibua kwa mara nyingine suala la viboko shuleni.
Serikali ilipiga marufuku viboko kwa wanafunzi shuleni mwaka 2001 lakini walimu wameonekana kuendelea kuvitumia kama njia ya kuadhibu wanafunzi.