Serikali imesema imejitolea kubuni mazingira mwafaka ya kufanya biashara, kuhakikisha sekta ya utengenezaji bidhaa inafaulu.
Waziri wa uwekezaji, biashara na viwanda Salim Mvurya, alisema wizarqa yake inajizatiti kuwezesha bidhaa zinazotengenezewa hapa nchini, zinaafikia viwango vya ubora vya kimataifa.
“Kama serikali, tunatambua jukumu linalotekelezwa na sekta ya utengenezaji bidhaa, kuanzia kwa biashara ndogo zinazokuza talanta za mashinani, hadi biashara kubwa, zinazopigia uvumbuzi wa Kenya katika majukwaa ya kimataifa.
Kulingana na waziri huyo, Kenya huzalisha bidhaa za ubora wa hali ya juu, huku raia wa taifa hilo wakijivunia kuwa ulimwengu mzima unatambua swala hilo.
Mvurya aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa tamasha la Changamka Kenya Shopping pamoja na kongamano kuhusu viwanda katika jumba la mikutano ya kimataifa,KICC.
Tamasha hilo limeqandaliwa kwa pamoja na muungano wa watengenezaji bidha na wizara ya biashara, kupiga jeki utengenezaji bidhaa na viwanda, ili kubuni ajira na uzalishaji wa mali.