Mvua ya Masika kuanza mapema kuliko ilivyotarajiwa

Judith Akolo
2 Min Read
Mvua ya Masika hapa nchini kuanza mapema.

Idara ya utabiri wa hali ya Hewa nchini, imesema kuwa msimu wa mvua za masika huenda ukaanza mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Idara hiyo imesema mvua hiyo itaanza mapema katika baadhi ya maeneo nchini kutokana na mfumo unaojulikana kama Madden Julianne Oscillation -MJO.

Haya ni mawingu yanayobeba mvua  ambayo hutembea katika bahari ya tropiki na kuleta mvua nchini. Athari hii ilionekana hapo awali katika awamu ya pili ya Madden Julianne Oscillation, inayotarajiwa katika wiki ya pili ya mwezi Machi na kusababisha kuanza kwa msimu huo mapema.

Utabiri wa hali ya hewa wa mwezi huu wa Machi  unaonyesha mvua inayozidi  wastani inatarajiwa kunyesha katika Bonde la Ziwa Viktoria, Nyanda za Juu Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ufa la Kati na Kusini, Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa, ikijumuisha Kaunti ya Nairobi, nyanda za chini za Kusini-Mashariki, na maeneo yaliyotengwa Kaskazini-Mashariki na Kaskazini-Magharibi.

Katika taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Hali ya Hewa Dkt David Gikungu, amesema mvua zinazokaribia kufikia chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Pwani, maeneo mengi ya Kaskazini Mashariki na Kaskazini Magharibi.

Alisema  kuwa hali ya joto inatarajiwa kuongezeka zaidi kuliko wastani kote nchini hasa katika maeneo ya Kaskazini-mashariki, Kaskazini-Magharibi, Nyanda za Juu Mashariki mwa Bonde la Ufa ikiwa ni pamoja na Kaunti ya Nairobi na sehemu za Pwani na nyanda tambarare za Kusini-mashariki

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *