Idara ya utabiri wa hali ya hewa hapa nchini imesema maeneo mengi yataendelea kushuhudia kiwango kikubwa cha mvua.
Kulingana na utabiri uliotolewa na idara hiyo wa siku saba zijazo, imvua kubwa itashuhudiwa husuan nyanda za juu mashariki ya Rift Valley, ziwa Viktoria, pwani, kaskazini magharii na kaskazini mashariki ya Kenya.
Naibu Mkurugenzi wa huduma za hali ya hewa Kennedy Thiong’o, alisema halijoto ya wastani wakati wa mchana ya zaidi ya nyuzi 30, itashuhudiwa pwani, kaskazini mashariki na kaskazini magharibi ya nchi huku halijoto wakati wa usiku ikishuka na kufikia nyuzi 10 kwenye maeneo kadhaa ya nyanda za juu mashariki ya bonde la ufa, eneo la kati la bonde la ufa pamoja na nyanda za chini za kusini mashariki.
Katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa nchi zikiwemo kaunti za Tukana na Samburu, mvua itashuhudiwa wakati wa asubuhi na alasiri, huku mvua na ngurumo za radi zikitarajiwa katika maeneo machache nyakati za usiku.
Aidha utabiri huo unaashiria kuwa eneo la pwani ikijumuisha Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale, yatashuhudia mvua nyakati za asubuhi na alasiri, maeneo kadhaa yakishuhudia mvua nyakati za usiku.