Muungano wa Azimio wafutilia mbali maandamano

Marion Bosire
2 Min Read

Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya umetangaza kufutiliwa mbali kwa maandamano ambayo yalikuwa yamepangwa kuandaliwa kesho Jumatano.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, muungano huo umeitisha maandamano kote nchini kulalamikia gharama ya juu ya maisha na kushinikiza kubatilishwa kwa sheria ya fedha ya mwaka 2023, maandamano ambayo yamekumbwa na vurugu tele.

Watu kadhaa wameripotiwa kufariki, wengine kujeruhiwa na mali ya mamilioni ya pesa kuharibiwa.

Ukifahamu athari za wito wake, muungano huo sasa umeewataka Wakenya kuandaa aina tofauti ya maandamano hiyo kesho. Umewataka kukesha ili kuwakumbuka na kutoa heshima kwa wote waliofariki wakati wa maandamano ya awali.

Kupitia taarifa, muungano wa Azimio ulidai Wakenya wapatao 50 wamefariki kwenye maandamano huku wengine wengi wakilazwa hospitalini wakiwa na majeraha mabaya.

Kulingana na taarifa, maandamano ya amani siku hiyo yatafanyika kwa njia tofauti kabisa ambapo magwaride ya mshikamano katika sehemu mbalimbali nchini yataandaliwa. Wananchi wanatakiwa kujitokeza kuwasha mishumaa na kuweka maua ikiwezekana ya rangi nyeupe ili kuwakumbuka waathiriwa.

Upinzani unadai hospitali zimetakiwa kutotoa taarifa kuhusu maafa yaliyotokana na maandamano na kwa sababu hiyo wengi wa waathiriwa wanauguza majeraha nyumbani, na iwapo vifo vinatokea nyumbani hakuna takwimu zake.

Muungano wa Azimio umedokeza kuwa una mipango ya kuzuru familia za waathiriwa na kuwapa usaidizi ili kuwapunguzia mzigo wa bili za hozpitali na gharama za mazishi.

Umeahidi kutoa orodha ya waathiriwa hivi karibuni.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *