Muungano wa Azimo la Umoja One Kenya, umewafurusha baadhi ya viongozi wake, kwa madai kwamba wameteuliwa serikalini au wanashirikiana na vyama au miungano hasimu ya kisiasa.
Kupitia kwa taarifa siku ya Jumatatu, baadhi ya wale waliofurushwa ni pamoja na Mawaziri Hassan Joho (Madini), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), James Opiyo Wandanyi (Nishati), Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed na mbunge mteule Sabina Chege.
Wengine waliotimuliwa ni Abdi Noor Farah, wabunge Adan Keynan (Eldas), David Pkosing (Pokot Kusini), Mishi Mboko (Likoni),Abdul Haji (Samburu Magharibi), Isabella Githinji, Caroline Karugu, na Solomon Kuria.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya kuandiliwa kwa mkutano wa Baraza Kuu na Baraza tekelezi la Kitaifa siku ya Jumatatu.
Wakati huo huo, muungano huo ulimteua Caroli Omondi kuwa kiongozi wake bungeni na hivyo kutamatisha hatamu ya Junet Mohammed kwenye wadhifa huo.
Muungano huo ulisema hivi karibuni utatangaza orodha ya viongozi watakaochukua nyadhifa zilizoachwa wazi.