Musalia Mudavadi ateuliwa kaimu Waziri wa Usalama wa Taifa

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri mwenye mamlaka makuu Musalia Mudavadi.

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ameteuliwa kuwa kaimu Waziri wa Usalama wa Taifa, wadhifa ulioshikiliwa na Prof. Kithure Kindiki ambaye sasa ni Naibu Rais mteule.

Kuteuliwa kwa Mudavadi, kunajiri saa chache baada ya tangazo kupitia gazeti rasmi la serikali kwamba Prof. Kindiki ataapishwa kesho Ijumaa kuwa Naibu Rais wa taifa.

Prof. Kindiki aliteuliwa kuwa Naibu Rais baada ya kuondolewa kwa Gachagua katika wadhifa huo.

Kulingana na gazeti hilo rasmi la serikali la Oktoba 31, 2024, Kindiki ataapishwa Novemba 1,2024 katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa la KICC kuanzia saa nne asubuhi.

Hatua hiyo ilijiri baada ya Mahakama Kuu kufutilia mbali agizo lililozuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki kuwa Naibu wa Rais.

Kulingana na Mahakama hiyo, kusalia wazi kwa afisi ya Naibu Rais kunakiuka baadhi ya sehemu za katiba ya nchi hii.

Maagizo ya kuzuia kuapishwa kwa Prof. Kindiki, yalitolewa na mahakama moja ya Kerugoya wiki mbili zilizopita punde tu baada ya Rais William Ruto kumteua Waziri huyo wa Usalama wa Kitaifa kuchukua mahali pa Gachagua.

Share This Article