Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen, amesema wizara yake itaunga mkono Chama cha Riadha nchini AK, kuandaa kambi za mafunzo kwa vijana wakati huu ambapo shule zimefungwa.
Akizungumza leo Jumatano alipozuru jumba la Riadha, waziri huyo alisema wadau wote wa riadha kutoka ngazi za taifa hadi mashinani, watajumuishwa kufanikisha mpango huo.
Murkomen alisema wizara yake itaongeza maradufu mgao wa bajeti kwa vyuo na kambi za vijana kote humu nchini ili kuboresha ukuzaji wa vipaji.
“Tunatekeleza mpango wa kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya michezo katika maeneo lengwa hapa nchini,” alisema Murkomen.
Pia alitangaza kuwa wizara yake inaunga mkono maombi ya Kenya ya kuandaa mashindano ya riadha ya Dunia mwaka 2029, akisisitiza kuwa amejitolea kuhakikisha kuwa viwanja vya Kasarani na Talanta vinakamilishwa kwa wakati ufaao ili kushirikishwa kwenye mchakato wa kuwania uandalizi.
Kenya itatoa ombi lake la pili baada ya kutofaulu katika majaribio yake ya kuandaa mashindano ya riadha duniani mwaka 2025 ambayo hatimaye yalikabidhiwa Tokyo, Japan.