Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, amesema kuwa visa vya ujangili na wizi wa mifugo vimepungua katika robo ya kwanza ya mwaka kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu.
Kulingana na waziri huyo, visa 167 vilinakiliwa katika kipindi hicho ikilinganishwa na visa 263 vilivyonakiliwa katika kipindi sawa na hicho mwaka 2024.
Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa X, Waziri huyo alisema mifugo 4,935 walioibwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ikilinganishwa na mifugo 8, 557 walioibwa katika kipindi sawa na hicho mwaka 2024.
Wakati huo huo, Murkomen alisikitikia vifo vya watu 21 kutokana na uhalifu kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu, ikilinganishwa na watu 58 waliouawa katika kipindi sawa na hicho mwaka 2024. Watu hao walijumuisha afisa mmoja wa polisi, raia 8 na washukiwa 12.
Murkomen alihusisha kupungua huko kwa visa vya uhalifu na ushirikiano mwafaka wa asasi za usalama wakiwmo maafisa wa polisi wa akiba (NPR).
Aidha, alisema kuna baadhi ya changamoto zinazodumaza juhudi za vikosi vya usalama za kuhakikisha usalama na utulivu ambazo zinajumuisha usambazaji wa silaha haramu ndogo ndogo, soko tayari la mifugo walioibwa, mwingilio wa kisiasa na uchochezi, ung’ang’aniaji wa lishe na maji nyakati za kiangazi, mzozo kuhusu mipaka ya ardhi, na ukosefu wa maficho kwa wahalifu kutokana na miundomsingi duni.
“Serikali inajizatiti kutenga rasilimali zaidi za maendeleo ya miundomsingi zikiwemo shule pamoja na vifaa bora kwa maafisa wa usalama kukabiliana na changamoto hizo,” alisema Murkomen.
Nawahimiza Wakenya kushirikiana kwa karibu na maafisa wa usalama tunapotia bidii kuhakikisha usalama hapa nchini,” aliongeza Waziri Murkomen.
Wakati huo huo alitoa wito kwa wanasiasa kuto-ingiza siasa katika maswala muhimu ya usalama wa Taifa.
Alisifu hatua zilizopigwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu akisema,”Tutatia bidii kulinda hatua hizo na kuhakikisha usalama mwaka mzima,”.