Murkomen: Uwanja wa ndege wa JKIA hautakosa umeme tena

Tom Mathinji
1 Min Read

Waziri wa barabara na uchukuzi Kipchumba Murkomen,  amehakikishia taifa kwamba hakutakuwa na tatizo la kupotea kwa umeme tena katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Tangazo hilo la Murkomen linajiri siku chache baada ya shughuli kusambaratishwa katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa, kutokana na kupotea kwa umeme katika sehemu kadhaa za nchi.

Akipokea ripoti ya kiufundi kutoka kwa maafisa wakuu wa kusimamia viwanja vya ndege na wale wa kusimamia safari za ndege, Waziri Murkomen alisema wamebadilisha vifaa vya kuwasha jenereta mara moja, umeme unapopotea.

“Viongozi wa KAA wamenihakikishia kwamba tatizo la kutokuwa na umeme katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa JKIA, halitakuwepo tena baada ya kuwekwa vifaa vya kuwasha jenereta mara moja umeme unapopotea,” alisema Murkomen.

Aidha, waziri Murkomen alisema vifaa mbadala vya kuwasha mitambo hiyo kwa mikono pia vimewekwa, vifaa vya kutambua hitilafu kuwekwa, nyaya zaidi za kusambaza kumeme kuwekwa na vifaa vya kubadilisha aina ya umeme unaotumika almaarufu inverters kuwekwa katika uwanja huo wa ndege ili kubadilisha aina ya umeme unaotumika katika muda wa sekunde 15.

Share This Article