Murkomen: Upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kerenga utaimarisha uchumi

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri Kipchumba Murkomen akagua ukarabati wa uwanja wa ndege wa Karenga kaunti ya Kericho.

Waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen, amepongeza ukarabati uanoendelea wa kupanua uwanja wa ndege wa Kerenga katika kaunti ya Kericho, akisema utakamilika kabla ya siku kuu ya Mashujaa.

Waziri alisema miundo msingi ni kichocheo cha maendeleo, na wizara yake itafanya kila iwezalo kutoa fursa za uwekezaji hapa nchini.

“Upanuzi unaoendelea wa uwanja huu wa ndege, utahudumia ndege zinazowabeba abiria hadi 37, lakini baadae utapanuliwa zaidi kuhudumia ndege za hadi abiria 60,”alisema Murkomen.

Murkomen aliyasema hapo alipokuwa akikagua ukarabati unaofanyiwa uwanja huo wa ndege, utakaotumika katika usafiri wa wageni watakaohudhuria sherehe ya Mashujaa katika uwanja wa Kericho Green tarehe 20 mwezi Oktoba.

Aidha alisema majaribio ya ndege kutua na kupaa yalifanyika siku mbili zilizopita, na kuongeza kuwa ndege ya Mama Taifa ilitua kwenye uwanja huo na kupaa baada ya hafla katika kaunti ya Kericho.

“Ninafuraha kudokeza kuwa majaribio ya kupaa na kutua kwa ndege yalifanikiwa na Mama Taifa Rachel Ruto, alikuwa wa kwanza kutua na kupaa kupitia uwanja huo siku ya Jumatano,”alisema Murkome.

Alisema uwanja huo utaimarisha usafiri na utalii katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na huduma za dharura za matibabu.

Gavana wa Kericho, Erick Mutai, na Mbunge wa Belgut, Nelson Koech, walipongeza serikali ya kitaifa kwa mradi huo, wakisema utakuwa na manufaa kwa mji wa Kericho na kuimarisha usafirishaji wa mizigo hadi maeneo mbalimbali.

Share This Article