Waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen, amesema ukuaji wa sekta ya uchukuzi wa ndege ni muhimu sana kwa serikali.
Waziri alitaja manufaa ya ukuaji huo kuwa ni pamoja na kubuniwa kwa nafasi za ajira, upanuzi wa masoko, kufanikisha usafirishaji wa bidhaa na watu, ukuaji wa chumi za kanda hii na kuifanya nchi hii kuwa kitovu cha uchukuzi wa ndege barani Afrika.
Akizungumza Jumatano wakati wa hafla ya kukabidhi ndege aina ya Boeing 737-700 kwa shule ya upili ya Mang’u, waziri alisema serikali inanuia kuleta ukuaji wa sekta ya uchukuzi wa ndege kwa kushirikiana na mashirika ya kiserikali, wadau wa sekta hiyo na shule katika kuanzisha vitovu vya ubunifu na ukuzaji vipaji na kutekeleza mikakati inayohimili mabadiliko ya hali ya anga.
Alisema kuwa hatua hiyo ya shirika la ndege la Kenya Airways ya kutoa ndege kwa shule, inaambatana na ajenda ya serikali ya kuleta mabadiliko kutoka viwango vya mashinani inayonuia kuwahusisha vijana na biashara ndogo ndogo na zile za kadri kubuni suluhu kwa changamoto zilizoko.
Aidha alidokeza kuwa hatua hiyo pia itasababisha ubunifu wa kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Alilishukuru shirika la ndege la Kenya Airways kwa kuunga mkono ukuzaji vipaji kupitia kitovu cha ubunifu katika sekta ya uchukuzi wa ndege cha fahari na chuo chake cha mafunzo ya uchukuzi wa ndege cha Pride Centre.