Murkomen: Serikali italinda taifa dhidi ya siasa za ghasia

Tom Mathinji
2 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen.

Serikali imesema itajizatiti kuhakikisha inalinda taifa hili dhidi ya siasa za uchochezi na ghasia.

Waziri wa Usalama wa Taifa  Kipchumba Murkomen,  amesisitiza uwajibikaji wa serikali akidokeza kuwa maafisa wa usalama watakabiliana vilivyo na wachochezi wa ghasia bila kujali hadhi  zao za kisiasa.

Akizungumza Ijumaa katika eneo bunge la Suba Kusini kaunti ya Homabay, Murkomen aliwashauri vijana kutotumiwa na wanasiasa kuzua vurugu wakati wa kampeni.

“Tumejitolea kulinda taifa hili dhidi ya siasa za uchochezi…tutakabiliana na vilivvyo na wachochezi kwa mujibu wa sheria bila kujali hadhi yao ya kisiasa,” alisema Murkomen.

Alikuwa akizungumza wakati wa shughuli ya kuwezesha kifedha makundi ya wanawake na ya wafanyabiashara katika kaunti ya Homa Bay akiwa ameandamana na Naibu Rais Kithure Kindiki.

Alisema mipango hiyo ya uwezeshaji inawiana na mikakati ya serikali inayolenga kuimarisha mapato katika maeneo ya mashinani.

Matamshi ya Murkomen yanajiri huku visa vya uvunjaji sheria vikishuhudiwa kwenye mikutano ya kisiasa katika siku za hivi karibuni hapa nchini.

Wengine waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na kiongozi wa chama cha ODM Oburu Oginga, Waziri wa Fedha  John Mbadi, mwenzake wa Utalii Rebecca Miano, Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, Makatibu wa Wizara  Raymond Omollo, Betsy Njagi, Ummi Bashir, Dkt. Bonface Makokha na Dkt.. Jane Imbunya.

Share This Article