Ni afueni kwa Mawaziri wanne waliohudumu katika Baraza la Mawaziri lililovunjwa na Rais William Ruto siku chache zilizopita.
Hii ni baada ya wao kuteuliwa tena kuhudumu katika Baraza Jipya la Mawaziri.
Waziri wa zamani wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen sasa ameteuliwa kuwa Waziri mpya wa Michezo. Atachukua nafasi ya Ababu Namwamba ikiwa uteuzi wake utaidhinishwa na bunge. Wizara ya Barabara na Uchukuzi ilitwikwa Davis Chirchir wakati Rais Ruto alipotangaza orodha yake ya kwanza ya mawaziri.
Dkt. Alfred Mutua pia ana kila sababu ya kutabasamu baada ya kuteuliwa kuwa Waziri mpya wa Leba, wadhifa ambao awali ulishikiliwa na Florence Bore. Dkt. Mutua awali alihudumu kama Waziri wa Utalii, wadhifa ambao sasa utashikiliwa na Rebecca Miano ambaye awali alihudumu kama Waziri wa Biashara.
Mwingine ambaye ameteuliwa na Rais Ruto kuwa Waziri katika Baraza Jipya ni Salim Mvurya ambaye awali alihudumu kama Waziri wa Madini. Mvurya sasa ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara huku wadhifa wake wa zamani ukikabidhiwa Hassan Joho.