Murkomen: Kupunguzwa kwa walinzi wa Muturi kunaambatana na sheria

Tom Mathinji
1 Min Read
Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen.

Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen amesema bado hajapokea malalamishi rasmi kuhusiana na madai ya aliyekuwa Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi kwamba walinzi wake wamepunguzwa.

Murkomen alikanusha madai kuwa kuondolewa kwa walinzi wa Muturi ni  hatua ya kisiasa, akidokeza kuwa swala hilo linapaswa kushughulikiwa na Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.

Wakati huo huo, Murkomen alifafanua kwamba kupunguzwa kwa idadi ya walinzi ni swala la kawaida hususan kwa watumishi wa umma wa zamani.

“Hili ni swala dogo ambalo linapaswa kushughulikiwa na Inspekta Jenerali wa Polisi. Iwapo litaletwa kwangu, nitalishughulikia kuambatana na sheria,” alisema waziri huyo.

“Huwa tunapunguza idadi ya walinzi wa watumishi wa umma punde tu wanapoondoka afisini. Ni swala la kawaida na hutekelezwa kwa wote, hata mimi binafsi ikiwa nitaondoka afisini,” aliongeza Murkomen.

Waziri huyo alisema maafisa hutekeleza majukumu kulingana na katiba, na sio shinikizo za kisiasa.

“Maafisa wa usalama hufanya kazi kuzingatia sheria na wala sio kutokana na shinikizo za kisiasa.”

Website |  + posts
Share This Article