Murkomen awasihi madereva kutahadhari msimu huu wa Krismasi

Martin Mwanje
1 Min Read

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen ametoa wito kwa madereva kuzingatia kanuni za usalama barabarani ili kuepusha kutokea kwa ajali wakati huu wa msimu wa Krismasi. 

Murkomen hasa amewataka madereva kuhakikisha wanalala vya kutosha na kuhakikisha wanaepukana na uchovu aliyoutaja kuwa chanzo kikuu cha ajali barabarani.

“Kabla ya kuanza safari, hakikisha unalala vya kutosha. Anza safari yako angalau saa moja baada ya kuamka,” Waziri Murkomen amewashauri madereva.

“Kwa safari ndefu zinazochukua siku kadhaa, dhamiria kusafiri kwa muda usiozidi zaidi ya saa 8 au 10 kila siku.”

Wamiliki wa magari ya masafa marefu ya usafiri wa umma wametakiwa kuhakikisha wana madereva wawili ili kuhakikisha mmoja anapumzika baada ya saa 10 za uendeshaji gari.

Matamshi yake yanakuja wakati kumetokea ajali kadhaa barabarani katika siku za hivi karibuni ambazo zimesababisha vifo vya watu zaidi ya 10.

Wengine wameachwa wakiuguza majeraha.

 

Share This Article