Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen ameshutumu na kuwaomba msamaha wanahabari na wanafunzi waliojipata taabani kufuatia vurugu zilizohusisha wanasiasa na polisi katika kaunti ya Nakuru.
Murkomen ametaja kuwa cha kusikitisha kile kilichowafika wanafunzi wa shule ya upili ya Butere katika Tamasha la Taifa la Michezo ya Kuigiza mjini Nakuru.
Pia ameahidi kulinda haki za uhuru wa kujieleza na vyombo vya habari akisema siyo dhamira ya serikali kukandamiza haki zao kama ilivyoelezwa kwenye katiba.
“Inasikitisha na naomba msamaha. Siyo dhamira ya serikali kushambulia au kumjeruhi mwanahabari yeyote au raia,” alisema Waziri huyo.
Huku akilaani tukio hilo, Murkomen ameapa kuwachukulia hatua maafisa wa usalama ambao huenda walitumia nguvu kupita kiasi kushughulikia suala hilo.
“Tunaenda kuchunguza na kubaini ikiwa tukio hilo lilifanyika kwa bahati mbaya au kimakusudi na kuchukua hatua,” aliahidi Waziri huyo.
Matamshi yake yanakuja saa chache baada ya polisi kuwafurusha wanahabari na wanafunzi wa shule ya wasichana ya Butere kutoka kwa Tamasha la Muziki, Sanaa na Maigizo awamu ya kitaifa linaloendelea katika ukumbi wa Melvin Jones, kaunti ya Nakuru.
Wanafunzi hao waliagizwa kuondoka ukumbini kutokana na mchezo wao wa kuigiza waliopanga kuwasilisha kwa kichwa “Echoes of War” kwa madai ya kuchochea uhasama.
Awali, chama cha ODM kimelaani vikali hatua ya serikali kuzuia wanafunzi wa shule ya wasichana ya Butere kutoka kaunti ya Kakamega kuwasilisha mchezo wao wa kuigiza wenye kichwa “Echoes of War.”
Wanafunzi hao walitarajiwa kuigiza mchezo huo wakati wa Tamasha la Taifa la Michezo ya Kuigiza linalofanyika mjini Nakuru.
“Nchi imetazama kwa kutoamini, kisa cha kusikitisha kwenye Tamasha la Taifa la Michezo ya Kuigiza mjini Nakuru ambapo serikali imeonekana kutia baridi kutokana na mchezo wa kuigiza wa shule ya upili ya wasichana ya Butere wenye kichwa, ‘Echoes of War’,” alisema Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna kwenye taarifa.
“Masuala nyeti yanaibuka wakati serikali inapoogopa sanaa ya watoto, hali tu ya kunadi kipaji katika tamasha la shule ya upili,” aliongeza Sifuna ambaye pia ni Seneta wa kaunti ya Nairobi.
Chama hicho aidha kimelaani vikali kudhulumiwa kwa shule ya upili ya wasichana ya Butere, wanahabari na watu wengine waliohudhuria tamasha hilo na kushinikiza kuwa shule ya Butere ikubaliwe kuwasilisha mchezo wake wa kuigiza.