Mugure Thande na David Majanja miongoni mwa majaji waliohamishwa

Tom Mathinji
2 Min Read

Idara ya Mahakama imewahamisha majaji 13 kupitia tangazo lililotolewa juzi Jumatatu.

Miongoni mwa majaji waliohamishwa ni pamoja na Mugure Thande, ambaye alikuwa akiongoza kitengo cha maswala ya sheria katika mahakama ya Milimani. Thande sasa atahudumu kama mkuu wa mahakama ya Malindi.

Jaji Chacha Mwita amehamishwa kutoka mahakama ya Miliman hadi  kitengo cha sheria, huku akitwikwa jukumu la kuongoza kitengo hicho.

Jaji David Majanja ambaye kwa sasa anasikiliza kesi kuhusu sheria ya fedha ya mwaka 2023 amehamishwa hadi kitengo cha kijamii.

Jaji Diana Kavedza ambaye alipandishwa cheo hivi maajuzi kuwa jaji wa Mahakama Kuu na alikuwa akisimamia mahakama ya Kahawa, amehamishwa kutoka mahakama ya Milimani hadi katika mahakama za Kibra na Kahawa.

Jaji Hedwig Ong’udi amehamishwa kutoka mahakama ya kikatiba na haki za binadamu ya Milimani na sasa ataongoza kitengo cha haki za binadamu katika mahakama kuu ya Nakuru.

Jaji Maureen Odero wa mahakama ya Milimani amehamishwa hadi Mahakama Kuu ya Nyeri.

Jaji Hillary Chemitei amehamishwa kutoka Mahakama Kuu ya Nakuru hadi Mahakama Kuu ya Malindi.

Jaji wa Mahakama Kuu ya Nyeri Florence Muchemi amehamishwa kusimamia mahakama Kuu ya Thika, huku jaji wa Mahakama Kuu ya Kisii Patriciah Gichohi akipelekwa katika Mahakama Kuu ya Nakuru.

Jaji Teresa Odera wa Mahakama Kuu ya Nakuru ataelekea katika Mahakama Kuu ya Kisii.

Jaji Peter Mulwa wa Mahakama Kuu ya Kiambu amehamishwa hadi kitengo cha biashara na ushuru katika mahakama ya Milimani kuchukua mahali cha Chacha Mwita.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *