Mudavadi, Raila kutoa taarifa kuhusu uenyekiti wa AUC

Kevin Karunjira
1 Min Read
Musalia Mudavadi na Raila Odinga kutoa taarifa ya pamoja kuhusu uwaniaji wa uenyekiti wa AUC

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi na aliyekuwa Waziri Mkuu  Raila Odinga leo Jumatano watatoa taarifa ya pamoja kuhusu hatua zilizopigwa katika uwaniaji wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC.

Kupitia kwa taarifa kutoka afisi ya Mudavadi, mkutano huo utaandaliwa katika afisi ya Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje, iliyoko katika makao makuu ya shirika la reli nchini kwenye barabara ya Haile Selassie.

Hatua hiyo inajiri baada ya  baraza kuu la AU kutangaza kuwa kanda ya Afrika Mashariki iwasilishe ombi la kuwania uenyekiti wa Umoja wa Afrika. Tangazo hilo lilitolewa Machi 15, 2024..

Kiongozi huyo wa chama cha ODM amehakikishia bara la Afrika kwamba yuko tayari kwa wadhifa huo wa kuimarisha bara hilo.

Baada ya kushiriki mazungumzo na Rais William Ruto na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni, Raila alisema safari yake ya kuwa mwenyekiti wa AUC imeanza, baada ya kuidhinishwa na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Raila pia amepata uungwaji mkono wa Zimbabwe, kufuatia mazungumzo ya pande mbili kati ya Rais  Emmerson Mnangagwa na Rais William Ruto.

Share This Article