Mudavadi, Waziri Mkuu wa Denmark wazungumzia usalama barani Afrika

Martin Mwanje
1 Min Read

Hali ya sasa ya amani na usalama barani Afrika ilikuwa kiini cha mkutano ulioandaliwa leo Jumatatu kati ya  Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Fredriksen. 

Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya aliwasili mjini Copenhagen mapema leo Jumatatu ambako anamwakilisha Rais William Ruto katika mkutano wa ngazi za juu kuhusu ushirikiano kati ya Denmark na Afrika.

Anasema wakati wa mkutano kati yake na Fredriksen, pia walijadili umuhimu wa usaidizi wa kimataifa kwa michakato mbalimbali ya kudumisha amani barani Afrika.

Kadhalika aliwasilisha ujumbe wa Rais Ruto kwa Waziri Mkuu huyo kabla ya kufanyika kwa Mkutano wa Ngazi za Juu kuhusiana na mtazamo mpya wa serikali ya Denmark wa kuimarisha ushirikiano na mataifa ya Afrika.

“Tuna shauku juu ya kuboresha ushirikiano kati ya Kenya na Denmark, na kutumia ipasavyo fursa zilizopo huku kukiwa na hali inayobadilika ya kiuchumi, kijamii na kisiasa duniani,” alisema Mudavadi baada ya mkutano huo.

Share This Article