Serikali imepongeza juhudi zinazotekelezwa na wanawake katika kuzuia mizozo kwa ustawi wa taifa hili.
Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, amesema ipo haja ya kusikiza sauti za wanawake katika kukabliana na hatari zinazoibuka, hususan usalama wa Mabadiliko ya Tabia Nchi, ambapo wanawake ndio huathirika zaidi.
Akizungumza katika maadhimisho ya 24 ya mkutano wa maazimio wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (NUSCR 1325), Mudavadi alisema tangu kukumbatiwa kwa UNSCR 1325, idadi ya wanawake wanaojumuishwa katika michakato ya usalama imeongezeka, sauti zao zikisikika katika utoaji maamuzi.
“Tunapaswa kujitolea upya katika kutekeleza ajenda ya wanawake, amani na usalama, ili kuhakikisha sauti za wanawake zinatekeleza jukumu muhimu katika michakato ya amani na kwamba wana rasilimali na uungwaji mkono unaohitajika,” alisema Mudavadi.
Mudavadi ambaye pia ni waziri wa mambo ya nje, alidokeza kuwa Barani Afrika, wanawake wametekeleza jukumu muhimu kutatua mizozo, kuhubiri amani na kujenga upya jamii.
Kwa upande wake, katibu katika idara ya jinsia Anne Wangombe, aliwapongeza wadau waliohudhuria mkutano huo, kwa kujitolea kwao kupigia debe usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake hapa nchini.
“Wakati wanawake na wasichana wanawezeshwa, jamii nzima hustawi, uchumi hunawiri, na mataifa hunakili ufanisi,” alisema Wangombe.