Mkuu wa Mawaziri Nchini Kenya Musalia Mudavadi, amesema uhusiano wa kidiplomasia wa Kenya unazidi kubuni fursa za ushirikiano kote duniani.
Akizungumza alipokutana na Balozi wa Ufilipino nchini Kenya Marie Charlotte G. Tang, Mudavadi alisema mazungumzo yao yalilenga kuimarisha ushirikiano wa pande mbili katika maswala yanayojumuisha usimamizi wa maswala ya ughaibuni, mafunzo ya majini na uchumi wa baharini.
Alisema sekta hizo ni muhimu kwa maendeleo ya ujuzi, kubuni nafasi za ajira hususan kwa vijana wa Kenya wanaotafuta ajira ughaibuni.
“Huku Ufilipino likiwa taifa bora kwa maswala ya baharini, Kenya itatumia fursa ya ushirikiano huu kupanua uwezo wake wa Uchumi wa Baharini,” alisema Mudavadi.
Alidokeza kuwa nchi hizo mbili zinajitahidi kubuni fursa mpya za kibiashara, uwekezaji na maendeleo ya nguvukazi.
Balozi huyo alikuwa akiwasilisha shukrani za nchi yake baada ya Kenya kuiunga mkono Ufilipino kwenye uwaniaji wa wadhifa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo Ufilipino haikupata nafasi ya kujiunga na baraza hilo baada ya kushindwa na Kyrgyzstan iliyopata kura 142 dhidi ya kura 49 za Ufilipino.