Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi anasema serikali inatathmini kwa kina mikakati kwa lengo la kuisadia nchi hii kujinadi yenyewe katika dunia ambayo kwa sasa inakumbwa na matatizo yanayoongezeka ya siasa za kimaeneo.
Kulingana naye, mikakati hiyo itatilia mkazo maongozi bora na ushirikishaji wa umma.
“Shabaha yetu ni kanuni thabiti za maongozi ya wazi na kushirikishwa kwa umma ili kuangazia mianya ya muda mrefu kati ya sera yetu ya kigeni na mahitaji ya maendeleo ya watu wetu,” alisema Mudavadi ambaye pia ni kinara wa mawaziri.
Aliyazungumza hayo alipokutana na wasomi na wataalam wa masuala ya kigeni ikiwa ni pamoja na mabalozi wastaafu, wakurugenzi wakuu na wakuu wa idara za Wizara ya Mambo ya Nje leo Jumanne.
Mkutano huo ulilenga kutafuta njia za kufanyia mapitio sera ya kigeni ya taifa hili.