Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amefanya mashauriano na mwenzake wa Ethiopia Balozi Taye Atseke-Selassie, ambapo walijadiliana kuhusiana na uimarishaji wa uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Katika mkutano huo uliofanyika siku ya Alhamisi Jijini Addis Ababa, Ethiopia, viongozi hao wawili pia walijadili kuhusu juhudi za kuleta amani na usalama katika upembe wa Afrika.
“Mazungumzo yetu yaliangazia maslahi ya nchi hizi mbili, pamoja na amani na usalama katika upembe wa Afrika,” alisema Mudavadi kupitia ukurasa wake wa X.
Huku wakijadili kuhusu uchaguzi ujao wa uongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC mapema mwaka ujao, Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ethiopia alimhakikishia Mudavadi kwamba taifa lake litamuunga mkono muwaniaji wa wadhifa wa mwenyekiti wa tume hiyo kutoka Afrika Mashariki.
Aidha, aliitaja Kenya kuwa mshirika mkuu wa Ethiopia na kuunga mkono azima ya Kenya ya kuwania uenyekiti wa AUC.
Wawili hao walikutana kabla ya kuandaliwa kwa mkutano wa 22 wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Mawaziri wa Mambo ya Nje Jijini Addis Ababa siku ya Ijumaa.