Katika hatua inayodhamiriwa kuimarisha ufanisi katika utendakazi wa umma, waziri aliye na mamlaka makuu ambaye pia ni waziri wa mashauri ya nchi za kigeni Musalia Mudavadi, amezuru afisi za idara ya uhamiaji.
Mudavadi alisema kwamba alitekeleza ziara hiyo katika jumba la Nyayo jijini Nairobi kujifahamisha.
Alishukuru wafanyakazi wa idara hiyo kwa mapokezi mema akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuafikia malengo ya uwazi, uwajibikaji na ubora katika utoaji huduma kwa umma.
“Ninatizamia ushirikiano ili kuafikia uwazi, uwajibikaji na ubora katika utoaji huduma kwa umma, masuala muhimu katika ufanisi wa taifa hili.” alisema Mudavadi.
Ziara yake inajiri wakati serikali inaangazia kuboresha huduma kwa umma katika idara mbali mbali na muda mfupi baada ya zoezi la kutia saini mikataba ya utendakazi ya mawaziri na makatibu katika ikulu ya Nairobi.
Katibu wa uhamiaji na huduma kwa wananchi Julius Bitok, alikuwa mwenyeji wa Mudavadi.