Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametoa wito kwa maafisa wa polisi na wale wa idara ya urekebishaji tabia kukuza uhusiano mzuri na raia kupitia mazungumzo yenye tija wanapokuwa kazini.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje amesema mazungumzo yanapaswa nyakati zote kupewa kipaumbele wakati wa kutatua migogoro kati ya maafisa wa polisi na raia.
Ameongeza kuwa kukuza mtamzamo wa pamoja na unaofaa kupitia mitazamo ya kimkakati itasaidia kuongeza ubora katika kuwahudumia raia.
“Tunapaswa kutafuta kuhamasisha uaminifu na uelewa utakaohakikisha usalama wa raia wetu, kuboresha mazingira ya biashara, na kuchochea mabadiliko ya kijamii na kiuchumi,” said Mudavadi.
“Tunapaswa kila wakati kulenga kutumia fursa zinazojitokeza ndani ya mipaka ya mazungumzo na raia na kukuza ushirikiano wa jamii uliojikita kwa utawala wa sheria, demokrasia na haki za binadamu.”
Mkuu huyo wa Mawaziri alikuwa akizungumza wakati wa uzinduzi wa mipango ya kimkakati ya Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS na Idara ya Urekebishaji Tabia katika Shule ya Mafunzo ya Serikali, KSG katika eneo la Lower Kabete, kaunti ya Nairobi.
Ameahidi kuwa serikali itaendelea kutoa usaidizi unaohitajika kwa maafisa mbalimbali wa usalama katika utendkazi wao.
“Ningependa kusisitiza dhamira ya serikali ya kuunga mkono NPS na Idara ya Urekebishaji Tabia kuongeza mipango inayotekelezwa ndani ya mamlaka yao na serikali iko tayari kutembea safari mpya na maafisa hao kama ilivyoelezwa chini ya mipango hiyo miwili ya kimkakati,” alisema Mudavadi.
“Ushirikiano na washikadau, ikiwa ni pamoja na jamii mnayohudumia, ni muhimu katika kutimiza matokeo yaliyokusudiwa katika mipango mipya ya kimkakati.”
Mudavadi alitoa wito kwa Wakenya kuunga mkono na kufanya kazi na Huduma ya Taifa ya Polisi na maafisa wengine wa usalama katika kukuza umoja, amani na uthabiti uliojikita kwenye ari ya ustawi wa taifa.