Kinara wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi amewasili mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa ziara rasmi nchini humo.
Punde baada ya kuwasili, Mudavadi alipokelewa na Balozi wa Kenya nchini Ethiopia George Orina na Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje wa Ethiopia Fisseh Shawul.
Wakati wa ziara hiyo, Mudavadi pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia wataongoza kikao cha Tume ya Pamoja ya 36 ya Ngazi ya Mawaziri, JMC kati ya Kenya na Ethiopia.
Makubaliano kadhaa yanatarajiwa kutiwa saini kwa lengo la kuboresha zaidi uhusiano wa pande mbili kati ya nchi hizo.
Balozi Shawul, alisema Kenya na Ethiopia, zimeunganishwa na utamaduni na lugha, ambazo ni muhimu sana katika ushirikano wa pande zote mbili.
Alisema nchi hizo mbili zimefanya kazi kwa pamoja katika sekta za usalama na amani, pamoja na kukabiliana na ugaidi na ulanguzi wa binadamu katika kanda ya Afrika Mashariki.
Ethiopia imesema imejitolea kushirikiana na Kenya katika sekta mbalimbali.