Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametoa wito kwa wanataaluma wa elimu kuangazia masuala muhimu yanayoathiri elimu ikiwemo migogoro, mabadiliko ya tabia nchi na athari ya teknolojia.
Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje alitaja hali inayotisha katika eneo la Sahel na maeneo mengine ya bara la Afrika ambako wanafunzi wanaokadiriwa kuwa milioni 100 hawaendi shuleni kutokana na migogoro inayoendelea.
Amewataka viongozi wa elimu kutafuta suluhu bunifu kwa changamoto zinazoikumba dunia.
Alikuwa akizugumza alipomwakilisha Rais William Ruto wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Dunia wa Shirikisho la Kimataifa la Walimu Wakuu (ICP) uliong’oa nanga humu nchini siku ya Jumanne.
Mudavadi alihoji namna viongozi wa elimu wanaweza wakakwepa hali ngumu ya kutoa elimu bora katika mazingira yenye changamoto kama hayo.
“Nini kitafanyika kwa maisha ya watoto hawa, ikizingatiwa kwamba athari za migogoro zinaweza zikadumu hadi miaka 40,” aliuliza Mudavadi.
“Tunakaribia kubuni kizazi kilichopotea, na lazima tutafute njia za kuhakikisha mustakabali wao hauko hatarini.”
Kadhalika, Mudavadi alizungumzia suala nyeti la mabadiliko ya tabia nchi.
Alitaja matukio ya hivi karibuni nchini Kenya ambako ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita uliharibu zaidi ya madarasa 4,000 pamoja na miundombinu muhimu kama vile madaraja na barabara zinazotumiwa kwenda shule.
“Ni lazima tutambue kuwa mabadiliko ya tabia nchi siyo tu suala la kimazingira, linaathiri moja kwa moja mifumo yetu ya elimu na fursa zilizopo kwa watoto wetu.”
ICP ilianzishwa mnamo mwaka 1990 na inaendelea kuhudumu kama jukwaa muhimu kwa mashirika ya uongozi wa shule duniani.
Shirikisho hilo linahamasisha uendelezaji na usaidizi wa viongozi wa shule katika mazingira mbalimbali ya elimu.