Mudavadi aishukuru UAE kwa kutoa nafasi za ajira kwa Wakenya

Tom Mathinji
2 Min Read

Waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, ameishukuru Muungano wa Milki za Kiarabu UAE, kwa kutoa nafasi 30,000 za ajira kwa raia wa Kenya.

Mudavadi, aliyepia waziri wa Mambo ya Nje, alielezea kujitolea kwa Kenya kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili pamoja na kupatikana kwa nafasi zaidi za ajira kwa wakenya walio na utaalam katika taifa hilo la Mashariki ya Kati.

“Ninaishukuru serikali ya UAE kwa nafasi nyingi za kazi ilizotoa kwa raia wa Kenya. Ninafuraha kwa sababu sasa wakenya 30,000 wanaishi na kufanya kazi katika taifa hili, wengi wao wakiwa katika sekta ya kazi za nyumbani,” alisema Mudavadi.

Akizungumza wakati wa kikao cha nne cha tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Kenya na UAE, Mudavadi alitoa wito kwa nchi hizo mbili kuharakisha utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano kuhusu leba wa mwaka 2018.

“Uhusiano huu umeendelea kuimarika hasaa katika maslahi ya pande zote mbili,” alisema Mudavadi alipotia saini mkataba wa maelewano  na waziri wa mambo ya nje wa UAE Shaikh Shakhboot Bin Nahyan Al Nahyan,  kuhusu ushirikiano wa pamoja katika maswala ya uongozi na Serikali.

Wakati huo huo Mudavadi alidokeza kuwa nchi hizo mbili ziko katika hatua za mwisho za kukamilisha mkataba wa ushirikiano katika maswala ya uchumi (CEPA), unaotarajiwa kutiwa saini wakati Rais wa UAE Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan,atakapozuru taifa hili kufuatia mwaliko wa Rais William Ruto.

“MKataba wa CEPA utaweka msingi kwa mataifa hayo mawili kuimarisha uhusiano wa kibiashara na uwekezaji, na ni matumaini yangu kwamba raia wa nchi hizo mbili watatumia fursa nyingi zitakazotolewa na mkataba huo,” alisema Mudavadi.

Mudavadi aliongeza kuwa juhudi zaidi zinapaswa kutekelezwa ili kuboresha zaidi uhusiano wa nchi hizo mbili, ili kuwawezesha raia wake kunufaika na fursa zilizopo.

Share This Article