Mudavadi ahakikishia walimu uungwaji mkono kutoka kwa serikali

Marion Bosire
2 Min Read

Waziri aliye na mamlaka makuu aliye pia waziri wa mambo ya nje Musalia Mudavadi amehakikishia walimu kwamba serikali imejitolea kuunga mkono ombi lao la kupata bima ya maisha ya pamoja kama sehemu ya bima yao ya matibabu.

Mudavadi alikiri kwamba walimu ndio watendakazi wa umma pekee wasio na bima ya maisha akisema serikali ya Kenya Kwanza imejitolea kuwaweka katika kiwango sawa na wahudumu wengine wa umma.

Akizungumza kwenye hafla ya kusherehekea miaka 25 ya chama cha KUPPET, waziri Mudavadi alisisitiza ushirikiano uliopo kati ya serikali na wadau katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.

Kuhusu changamoto zinazokumba walimu wa sekondari msingi wanaohudumu kwa kandarasi, Mudavadi aliahidi kujitolea kwa serikali kuboresha masharti yao ya kikazi kulingana na mapatano yao ya kuajiriwa.

“Mabadiliko ya haraka katika teknolojia, uchumi na jamii kote ulimwenguni, yanabadili jukumu la serikali katika masuala ya kutetea wafanyakazi” alisema Mudavadi akiongeza kwamba wanatambua pendekezo la KUPPET kuhusu zinakostahili kuwa shule za sekondari msingi.

Kando na hayo, waziri Mudavadi alizungumzia mipango inayotekelezwa na serikali kubadilisha sekta ya elimu ambayo imetengewa fedha zaidi kwenye bajeti kufadhili mipango kama uajiri wa walimu elfu 58.

Hatua hiyo alisema inalenga kukidhi hitaji lililopo la walimu 116,000 kufikia mwaka ujao wa kifedha.

Tume ya kuajiri walimu nchini TSC imepandisha vyeo walimu elfu 51, pia kwa lengo la kuboresha uwezo wa sekta ya elimu ili kuhakikisha matokeo bora.

Taasisi za masomo ya kiufundi almaarufu TVETs pia ziliongezewa ufadhili kutoka kwa serikali ili kuhakikisha zinakuwa kiung muhimu kwa wanaokamilisha elimu ya shule za msingi na shule za sekondari.

Wanafunzi wa familia maskini, Mudavadi alisema wanapata usaidizi wa kulipia masomo kutoka kwa serikali huku serikali ikiongeza pesa inazolipia kila mwanafunzi kwa lengo la kuhakikisha shule zinamudu gharama ya juu ya utoaji huduma.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na maafisa kadhaa wakuu serikalini na wale wa chama cha KUPPET, akiwemo mwenyekiti Omboko Milemba na katibu mkuu Akelo Misori.

Share This Article