Serikali imeongeza muda wa kutuma maombi ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne, KCSE wa mwaka 2023 wanaojiunga na vyuo vikuu mwaka huu.
Muda huo umeongezwa hadi tarehe 15 mwezi huu wa Agosti.
Kwenye taarifa, Katibu wa Elimu ya Juu Dkt. Beatrice Muganda alisema kuwa wanafunzi watafadhiliwa kuambatana na hitaji la kila mmoja chini ya mfumo mpya wa ufadhili wa masomo.
“Kuanzia tarehe 19 mwezi huu wa Agosti, wazazi na walezi wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu watajulishwa kiwango cha karo watakachohitajika kulipa,” alisema Muganda.
Dkt. Muganda alisisitiza kwamba ufadhili wa serikali wa masomo utatolewa tu kwa watakaotuma maombi ya ufadhili huo.
Mamlaka ya kutoa nafasi kwa wanafunzi katika vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu nchini (KUCCPS) imewasajili wanafunzi wapatao 153,275 waliofanya mtihani wa KCSE mwaka jana kujiunga na vyuo vikuu nchini.
Wizara ya Elimu ilitoa mwaliko kwa wanafunzi kutuma maombi ya ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vikuu mnamo tarehe 18 mwezi Juni mwaka huu.