Muda wa kutuma maombi ya kujiunga na vyuo vikuu na vyuo warefushwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Ni afueni kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne, KCSE mwaka jana baada ya serikali kuongeza muda wa kutuma maombi ya kujiunga na vyuo vikuu na vyuo nchini. 

Muda huo uliopaswa kukamilika kesho Jumanne, Februari 26 sasa umeongezwa kwa siku saba hadi Machi 4, 2024.

Katika taarifa, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu anasema hatua hiyo imetokana na ukweli kwamba ni asilimia 70 ya watahiniwa wanaotaka kujiunga na vyuo vikuu na vyuo waliofanikiwa kutuma maombi kufikia leo Jumatatu.

“Kufikia Februari 25, 2024, jumla ya watahiniwa 121,391 waliopata Gredi ya C+ na zaidi katika mtihani wa KCSE 2023 walikuwa wametuma maombi ya kufanya kozi mbalimbali. Hii ni asilimia 60.8 ya wanafunzi 199,695 waliopata Gredi ya C+ na zaidi katika mtihani wa 2023,” alisema Waziri Machogu.

“Kwa kuzingatia mwenendo wa utumaji maombi wa watahiniwa wa mwaka 2023 waliopata Gredi ya C+, inakadiriwa kwamba asilimia 86 ya watahiniwa wa KCSE 2023 waliopata Gredi ya C+ na zaidi “171,738” watatuma maombi.”

Makadirio ambayo yameifanya Wizara ya Elimu kuiagiza Mamlaka ya Kuwaweka Wanafunzi katika Vyuo Vikuu na Vyuo, KUCCPS kurefusha muda wa utumaji maombi hadi Machi 4, 2024.

Awali, KUCCPS ilirefusha muda huo kutoka Februari 22 hadi Februari 26, 2024 ila idadi ya watahiniwa waliotuma maombi bado si ya kuridhisha.

Kumekuwa na madai kuwa mtandao hafifu wa KUCCPS umechangia idadi ndogo ya watahiniwa wanaotuma maombi ya kujiunga na vyuo vikuu na vyuo, kwani mtandao huo haufunguki kwa urahisi.

 

Website |  + posts
Share This Article