Muda wa kuomba ufadhili wa elimu ya juu waongezwa

Marion Bosire
2 Min Read

Wizara ya elimu nchini Kenya imeongeza kwa mwezi mmoja zaidi muda wa kutuma maombi ya ufadhili wa elimu ya juu. Wanaotaka ufadhili katika mwaka 2023/2024 wana muda hadi Oktoba 7, 2023 kutuma maombi. Awali tarehe ya mwisho ilikuwa Septemba 7 2023.

Waziri wa elimu Ezekiel Machogu alisema katika taarifa kwamba hatua ya kuongeza muda wa kutuma maombi hayo, itahakikisha wanafunzi wote waliohitimu kujiunga na vyuo vikuu wanajiunga navyo.

Machogu alitangaza rasmi pia kwamba hitaji la kitambulisho cha kitaifa limeondolewa katika mchakato wa kutuma maombi ya ufadhili huo wa elimu kwa wanafunzi ambao hawajatimiza umri wa miaka 18.

“Kulingana na maelekezo ya baraza la mawaziri ya Agosti 29 2023, wizara ya elimu imeondoa hitaji la kitambulisho cha kitaifa kwa wanafunzi ambao hawajatimiza umri wa miaka 18 ili kuwapa fursa ya kutuma maombi ya ufadhili wa elimu.” alisema Machogu kwenye taarifa hiyo.

Alielekeza pia hazina ya vyuo vikuu na bodi ya ufadhili wa elimu ya juu HELB kuweka mikakati ya kurahisisha na kuharakisha mchakato wa kutoa ufadhili kwa wanafunzi wote.

Hazina hizi zimetakiwa kuweka watendakazi wao kwenye vituo vyote vya Huduma nchini kusaidia wanafunzi wanatuma maombi ya ufadhili wa elimu ya juu.

Wizara ya elimu inasema kufikia Septemba 5 2023, wanafunzi 156,532 walikuwa wametuma maombi ya ufadhili kwa hazina hizo mbili hiyo ikiwa asilimia 60 pekee ya wanafunzi waliopata nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu nchini.

Wengine 265,000 bado hawajatuma maombi ya ufadhili huo.

Share This Article