Muda wa kikosi cha jumuiya ya Afrika Mashariki DR Congo waongezwa

Marion Bosire
2 Min Read

Viongozi wa nchi za Afrika Mashariki walikubaliana Jumanne kuongeza muda wa kuhudumu wa kikosi cha eneo hili kilichotumwa mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC kutuliza hali.

Nchi saba za eneo hilo, wanachama wa jumuiya ya Afrika Masharik, zilituma vikosi vyao mashariki mwa DRC mara ya kwanza Novemba 2022 baada ya kuchipuza tena kwa kundi la waasi la M23.

Taarifa ya jumuiya ya EAC iliyotolewa baada ya kongamano jijini Nairobi Jumanne ilisema kwamba viongozi wa nchi hizo wamekubaliana kuongeza muda wa kikosi cha EACRF hadi Disemba 8, ikisubiriwa ripoti ya utathmini.

Hali ya kikosi hicho cha pamoja nchini Congo imekuwa ikitiliwa shaka hasa baada ya Rais wa DR Congo Felix Tshisekedi kukikosoa lakini EAC iliamua mwezi Juni kukiacha kikosi hicho nchini humo kwa miezi mitatu zaidi.

Makundi mengi yaliyojihami huvamia eneo la mashariki la nchi ya DR Congo lililo na madini mengi hasa miaka ya 1990s na 2000s.

Kundi la M23 linaloongozwa na wa – Tutsi limenyakua sehemu za mkoa wa Kivu Kaskazini tangu kurejea tena mwisho wa mwaka 2021.

Kikosi cha EAC kimefanikiwa kukomboa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakikaliwa na kundi la M23 lakini hakijafanikiwa kuzima maasi ya kundi hilo kabisa.

DR Congo inalaumu jirani yake Rwanda, ambayo pia ni mwanachama wa jumuiya ya EAC kwa kuunga mkono waasi madai ambayo Rwanda inakanusha.

Marekani na nchi kadhaa za Magharibi na hata wataalamu huru wa umoja wa mataifa wameafikia kwamba Rwanda inaunga mkono waasi nchini Congo.

Website |  + posts
Share This Article