Sasa imebainika kuwa mtu mmoja alifariki wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024.
Maandamano hayo jana Alhamisi yalishika kasi katika miji mbalimbali ikiwa ni pamoja na Nairobi, Nakuru, Eldoret, Kisumu, Mombasa na Kakamega.
Wakati wa maandamano hayo, polisi walionekana wakiwarushia waandamanaji, wengi wao vijana, vitoza machozi hasa Nairobi ili kuwatawanya licha ya waandamanaji kuonekana kudumisha amani.
Kiasi kwamba Mamlaka ya Kusimamia Utendakazi wa Polisi nchini, IPOA inasema imebaini kuuawa kwa mwandamanaji mmoja kwa jina Rex Masai anayedaiwa kufyatuliwa risasi na polisi wakati wa maandamano hayo.
“Mamlaka inawapongeza waandamanaji kwa kufanya maandamano ya amani huku wakiwa hawana silaha na pia kupongeza Huduma ya Taifa ya Polisi kwa kuonekana kujizuia kinyume cha maandamano ya awali,” alisema mwenyekiti wa IPOA Anne Makori katika taarifa.
“Hata hivyo, Mamlaka imerekodi kifo cha Bw. Rex Masai anayedaiwa kufariki baada ya kufyatuliwa risasi na polisi na waandamanaji wengine kadhaa kujeruhiwa vibaya wakiwemo maafisa wa polisi.”
Makori anasema IPOA imeanzisha uchunguzi kuhusiana na kupigwa risasi hadi kuuawa kwa Bw. Masai na kwamba timu yake ya uchunguzi tayari imewasiliana na familia ya marehemu.
Visa vya waandamanaji wengine kujeruhiwa vibaya wakati wa maandamano hayo pia vinachunguzwa.