Mwanaharakati mmoja wa haki za binadamu nchini Iran anayefahamika sana amejitoa uhai kulalamikia kile alichokitaja kuwa udikteta wa kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.
Katika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, Kianoosh Sanjari alisema kwamba angejitoa uhai iwapo wafungwa wa siasa hawangeachiliwa huru kufikia saa moja jioni, saa za nchi hiyo.
Kifo chake kilidhibitishwa saa chache baadaye na wanaharakati wenza.
Katika ujumbe mwingine wa awali, Sanjari alisema anatumai kwamba siku moja raia wa Iran wataamka na kukataa utumwa.
Alifahamika sana kwa kukosoa viongozi wa Iran na kutetea demokrasia na alisema hakuna mtu anafaa kufungwa kwa kutoa maoni na kwamba maandamano ni haki ya kila raia wa Iran.
Jamaa huyo alitaja wafungwa wanne waliokamatwa kwa kuunga mkono na kuhusika katika maandamano yaliyotokana na kifo cha Maahsa Amini cha mwaka 2022 baada ya kuzuiliwa na polisi wanaosimamia maadili.
Sanjari mwenyewe alikamatwa mara kadhaa kutokana na uanaharakati wake wa kisiasa kati ya mwaka 1999 na 2007.
Aliondoka Iran mwaka 2007 akapatiwa hifadhi huko Norway, kabla ya kujiunga na kampuni ya uanahabari ya Voice of Americ jijini Washington DC.
Mwaka 2016 alirejea Iran kukaa na wazazi wake akakamatwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 11 katika jela inayofahamika kuhifadhi wafungwa wa siasa.
Aliachiliwa kwa dhamana kwa sababu ya matatizo ya kiafya mwaka 2019 akapelekwa kwenye hospitali ya matatizo ya akili.