Mtangazaji mkongwe akamatwa Australia kwa makosa ya kufanya mapenzi

Marion Bosire
2 Min Read
Allan Jones

Mtangazaji mkongwe wa Australia ambaye pia aliwahi kuwa kocha wa raga Alan Jones amekamatwa kufuatia uchunguzi uliofanywa kuhusu madai ya makosa ya kufanya mapenzi.

Makosa hayo yanadaiwa kutekelezwa katika kipindi cha miongo miwili.

Jones wa umri wa miaka 83, amekuwa mtangazaji nchini Australia tangu miaka ya 1980, ambapo alikuwa anaongoza vipindi vyenye ushawishi katika vituo vya redio vya 2GB, 2UE na runinga ya Sky News.

Anafahamika kwa maoni yake ya kihafidhina na kabla ya kujiunga na utangazaji, alifanya kazi kama mwalimu kisha akaingilia siasa.

Katika ulingo wa siasa alikuwa anafanya kazi kama mwandishi wa hotuba na mshauri wa aliyekuwa waziri mkuu wa Australia Malcolm Fraser.

Kati ya mwaka 1984 na 1998, Jones alikuwa kocha mkuu wa timu ya Raga ya wanaume ya Australia ambapo alipata ushindi mara 86 katika mechi 102 .

Katika taarifa Jumatatu polisi wa jimbo la New South Wales walisema kwamba wapelelezi wa kundi maalum la kukabiliana na unyanyasaji wa watoto walikamata mwanaume wa miaka 83.

Kulingana na polisi hao, kukamatwa huko kunafuatia kubuniwa kwa kikosi mwezi Machi cha kuchunguza dhuluma za kingono zilizotokea mwaka 2001 hadi 2019.

Maafisa wa polisi hawakumtaja mshukiwa aliyekamatwa.

Disemba mwaka jana, Jones alikanusha makosa ya unyanyasaji na kupapasa visivyo baada ya gazeti la Sydney Morning Herald kuchapisha taarifa kuhusu uchunguzi uliobainisha kwamba alitumia wadhifa wake kuvizia wanaume wa umri mdogo.

Wakili wa Jones wakati huo alitaja madai dhidi ya mteja wake kuwa ya kikashfa, ya kukera na ya kumharibia jina.

Share This Article