Mswada wa kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi wapingwa

Tom Mathinji
2 Min Read

Huku bunge la Seneti linapojiandaa kujadili mapendekezo ya kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi waliochaguliwa, Askofu Mkuu wa kanisa la kianglikana hapa nchini Jackson Ole Sapit, ameonya kuhusu kupitishwa kwa mswaada huo na bunge la Senate.

Kulingana na Ole Sapit, mdahalo wa kuongeza muhula wa kuhudumu wa viongozi waliochaguliwa, unapaswa kushughulikiwa kupitia kura ya maoni.

Seneta wa Nandi Samson Cherargei, aliwasilisha mswada katika bunge la Seneti akioendekeza kuongezwa kwa muhula wa viongozi waliochaguliwa, kutoka miaka mitano hadi miaka saba,.

Kulingana na Cherargei, mswaada huo unadhamiriwa kumpa muda wa kutosha rais aliyechaguliwa na viongozi wengine kukamilisha miradi ya maendeleo.

Aidha mswada huo umepata upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi, huku Seneta wa kaunti ya Kiambu Karungo Thang’wa, akipendekeza muda huo upunguzwe kutoka miaka mitano hadi miaka minne.

Thang’wa anadai kuongezwa kwa kipindi cha kuhudumu hadi miaka saba kutatoa fursa ya uongozi wa kiimla na kutishia demokrasia.

Matamshi ya Thang’wa yanaungwa mkono na kiongozi wa wengi katika bunge la kitaifa Kimani Ichung’wa, ambaye kupitia mtandao wake wa X, alipuzlia mbali pendekezo hilo la kuongeza muhula wa kuhudumu, akisema mswaada huo kamwe haungepita.

Ichung’wa badala yake amemtaka Seneta  Cherargei kukoma kuwapotezea muda maseneta wenzake na wakenya kwa ujumla.

Wakenya wana hadi kesho Ijumaa, kuwasilisha maoni yao kuhusu mswaada huo ulio mbele ya bunge la seneti.

Mnamo siku ya Ijumaa tarehe 25 mwezi huu, kamati ya bunge la seneti kuhusu masuala ya sheria na haki za kibinadamu, itaandaa kikao cha kupokea maoni ya umma kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba, ambao miongoni mwa masuala mengine, unapendekeza kuongezwa kwa muda wa kuhudumu wa viongozi waliochaguliwa wakiwemo Rais na wabunge kutoka miaka mitano hadi miaka saba.

Share This Article