Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini kimeunga mkono kile kinachokitaja kuwa maandamano ya amani yanayofanywa na Wakenya kupingwa Mswada wa Fedha 2024.
Katika taarifa, chama hicho kinachoongozwa na Julius Malema kinasema maandamano yanayorindima humu nchini ni ishara tosha kwamba watu wanakataa sera zinazozidisha kuteseka kwao na kutaka kuwepo kwa serikali inayojali maslahi yao.
Aidha, kimetoa wito kwa maafisa wa polisi kutowakandamiza waandamanaji ambao kinasema kwa kiwango kikubwa wamedumisha amani.
“Tunalezea zaidi mashaka juu ya ukandamizaji wa waandamanaji wanaodumisha amani ambao umesababisha kujeruhiwa kwa watu wasiopungua 200 na zaidi ya 100 kukamatwa. Utumiaji wa vitoza machozi, mabomba ya maji na risasi za mpira dhidi ya raia wanaotekeleza haki yao ya kulalamika haukubaliki,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa ya EFF inakuja wakati ambapo msemaji wa serikali Isaac Mwaura amewataka vijana kushiriki mazungumzo na serikali ili kuangazia malalamishi yao na kujiepusha kutumiwa na watu kutoka nje ya nchi walio na nia ya kuvuruga amani humu nchini.
Katibu Mkuu wa chama cha UDA Cleophas Malalah pia amedai kuwa maandamano yanayoshuhudiwa nchini yanachochewa na watu kutoka nje ya nchi wenye nia ya kuvruga uthabiti wa nchi.
Vijana maarufu kama Gen Z wameapa kuendelea na maandamano yao hadi serikali iangazie malalamishi yao.